Ticker

6/recent/ticker-posts

NG'OMBE ANAWEZA KUTOA MAZIWA MENGI KAMA UKIZINGATIA MAMBO HAYA:

                          

Ukiachana na maandalizi mazuri ya ng'ombe wa maziwa akiwa mdogo ( ndama) kwa ajiri ya uzalishaji mzuri wa maziwa pia kuna mbinu nyingine zinazohitajika pale ng'ombe anapoanza kutoa maziwa ili kuongeza uwingi wa maziwa kwa ufanisi zaidi.

Ili ng'ombe atoe mziwa mengi pia zinahitajika jitihada za kutosha haswa kwenye chakula na matunzo ili aweze kutoa maziwa mengi kama uwekezaji wa aina yoyote ile. Pia ukiachana na malisho ya kijani ambayo ni chakula kikubwa cha ng'ombe ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo Ili kuboresha uzalishaji wa maziwa kwa ng'ombe wako kama ifautavyo.

1. Maji safi ya kutosha

2. Malisho bora ya kutosha

3. Chakula cha ziada ( Concentrate)

4. Madini kila siku

5. Kustarehe ( Comfort)

6. Kubadili chakula taratibu

7. Ukamuaji mzuri wa maziwa

 

1. Maji safi ya kutosha

                                     


Kiasi cha maji anachotakiwa kunywa ng'ombe kulingana na uzito wake ni kikubwa ukilinganisha na virutbisho vingine kama vile wanga (carbohydrates), protini (protein), madini (minerals) na mafuta (fats) ambavyo vinahitajika kwenye mlo wake, ambapo anatakiwa kunywa maji asilimia 75 ya uzito wake. Lakini wafugaji wengi wanaweka msisitizo kwenye sehemu kavu ya chakula (Dry matter) ambayo ni asilimia 25 tu ya virutbisho vyote anavyotakiwa katika mlo wake.

Ng'ombe anahitaji lita 1 ya maji kwa kila kilo 12 za uzito wake kipindi cha ubaridi na lita moja ya maji kwa kila kilo 6 ya uzito wake kipindi cha joto, kwa mfano kama ng'ombe ana kilo 300 anatakiwa kunywa maji lita 25 kwenye hali ya hewa ya ubaridi na lita 50  kwenye hali ya hewa yenye joto.

Kwa ng'ombe anaenyonyesha au anaetoa maziwa (lactating cow) mahitaji ya maji yanaongezeka mara mbili ya ng'ombe wa kawaida, pia umri wa ng'ombe, ukubwa wa mwili, hatua ya uzalishaji pamoja na mazingira yana amua kiasi cha maji kinachohitajika kwa siku.

Ni vizuri ng'ombe wa maziwa akipatiwa maji mara 4 mpaka 6 kwa siku ili kuongeza uzalishaji wa maziwa, kwani husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa ng'ombe. Chanzo cha maji kinashauriwa kisiwe mbali na makazi ya ng'ombe kwani ng'ombe hupoteza nishati nyingi kutembea kufuata maji ambapo hiyo nishati ingeweza kutumika kutengeneza maziwa. Kwa kila lita 5 ya maji anayokunywa ng'ombe inatakiwa kutoa angalau lita moja ya maziwa.

Pia ubora wa maji unatakiwa uangaliwe kwa hali ya juu kwa sababu maji mengine huwa na kiwango cha madini kilichopitiliza hivyo huathiri mmeng'enyo wa virutbisho (nutrients digestion) na uwiano wa madini kwa ng'ombe. Hivyo huathiri uzalishaji wa maziwa. Hivyo ni muhimu kujua kiwango cha madini kilichopo kwenye maji ambayo hupatiwa ng'ombe ili kuimarisha uzalishaji wa maziwa.

2. Malisho ya kutosha (feeds)


                    


Ili kuongeza uzalishaji wa maziwa, ng'ombe wa maziwa anatakiwa alishwe sehemu kavu (dry matter)ya kutosha  kama vile nyasi au majani makavu ( hay) au silaji ( silage). Hii ni kwa sababu vijidudu ( microbes) wanaopatikana katika rumen ya wanyama wote wanaocheua hawafanyi kazi kwa ufanisi haswa kwenye malisho yenye nyuzinyuzi ambayo hayajachachushwa ( fermented). Kwahiyo nyasi zilizokaushwa ( hay) au silaji ( silage) tayari zimechachushwa nje ya tumbo kwahiyo inakuwa rahisi kumeng'enywa yanapoliwa na kutumiwa haraka na mwili kuongeza utoaji wa maziwa kwa ng'ombe.

Kwahiyo ni vizuri kuhakikisha ng'ombe wa maziwa anakula malisho yenye mchanganyiko wa majani makavu kwa wingi na mabichi  kwa ajiri ya kumfanya awe na afya njema na kuzalisha maziwa mengi.

Pia ni muhimu kuzingatia ubora wa malisho kama vile malisho ya kijani yanatakiwa yawe machanga na yawe na rangi ya kijani kibichi yasiwe na matawi mengi kwani huwa na virutbisho vingi ukilinganisha na majani yaliyopoteza rangi yake ya ukijani, yaliyokomaa na yenye matawi mengi. Majani yakiwa yamekatwa katwa kwenye vipande vidogo vidogo ( Chopped grasses) yanapendeza zaidi.Pia majani jamii ya mikunde ni muhimu sana kwa ng'ombe wa maziwa kwani yana protini nyingi ukilinganisha na majani ya kawaida.

Mfugaji wa ng'ombe wa maziwa anatakiwa awe na chakula cha kutosha ( Food reserve) ambapo itamsaidia kumbadilishia ng'ombe wake vyakula tofauti tofauti kwa kufuata utaratibu maalumu Ili ng'ombe waendelee kutoa maziwa ya kutosha mda ote.

3. Kutengeneza chakula cha ziada chenye uwiano sahihi (Concentrate)

Kwa kawaida chakula kikuu cha ng'ombe ni nyasi na majani mabichi na makavu, lakini hakitoshi kumpa ng'ombe wa maziwa virutubisho muhimu hivyo inatakiwa apewe chakula cha ziada (Concentrate). Chakula cha ziada humpa ng'ombe virutubisho muhimu anavyohitaji kila siku. Ili ng'ombe aweze kutoa maziwa mengi ni muhimu kumpa chakula chenye lishe kwa kuchanganya vyakula vyenye wanga, protini, vitamini na madini, kwani hufanya ng'ombe apate virutubisho vya muhimu na vya ziada kwa ajiri ya kuongeza uzalishaji wa maziwa. Na lengo kuu la kumpa ng'ombe vyakula vyenye lishe ni kuongeza uzalishaji wa maziwa, ng'ombe anahitaji chakula cha ziada mbali na nyasi ambazo mara nyingi hufanya matumbo yao kujaa haraka bila kupata viini rishe vya kutosha.

Chakula cha ziada ( Concentrate) huwapa ng'ombe wako virutubisho vya kutosha kwa haraka ulikinganisha na nyasi za kawaida lakini chakula hiki kina gharimu kiasi kikubwa cha pesa, kwahiyo ni muhimu kuhakikisha kuwa ongezeko la maziwa linatosha kulipa gharama ya chakula kilichoonhezeka kutumika. Ni vizuri ukiwapa ng'ombe chakula cha ziada kuanzia kilo 2 hadi 4 asubuhi na jioni kwa ajiri ya kuongeza uzalishaji wa maziwa.

4. Hakikisha ng'ombe anapewa madini kila siku

Kuna aina tofauti tofauti za chumvi kwa ajiri ya aina tofauti ya wanyama, Ng'ombe wa maziwa wanahitaji madini kwa ajiri ya uzalishaji mkubwa wa maziwa, hivyo virutubisho vya kalsiamu (Calcium) na fosforasi (Phosphorus) ni muhimu sana kwa ng'ombe wa maziwa.

Malisho ya ng'ombe peke ake hayawezi kuwa na madini ya kutosha yatakayomnufaisha ng'ombe wa maziwa kwahiyo ni vizuri kuongezea chakula (feeds) madini yenye ubora wa hali ya juu kwa kuwapa jiwe la chumvi na kuhakikisha ng'ombe anayapata kila siku kwa ajiri ya kuongeza uzalishaji wa maziwa.

5. Hakikisha ng'ombe wanapumzika vya kutosha

Ng'ombe wa maziwa anantakiwa awekwe kwenye mazingira mazuri kama vile sakafu iliyosafishwa vizuri, kavu na  isiyoteleza kwani sakafu inayoteleza huatarisha afya ya ng'ombe ikiwa na mchanganyiko wa kinyesi pamoja na mikojo kwani ng'ombe wanaweza kuteleza, zizi la ng'ombe liwe na kivuli cha kutosha na liwe na hewa ya kutosha. Ng'ombe anapopata mda wa kutosha wa kupumzika na kucheua, huongeza mtiririko wa damu katika kiwele ( Udder) ambapo husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa. Kadri ng'ombe anapokosa mda wa kupumzika ( Lying down) ndivyo anavyozidi kupunguza uwezo wa kutoa maziwa mengi. Kwani ng'ombe wa maziwa anahitaji kupumzika masaa 10 mpaka 14 kwa siku ambapo anatumia masaa 7 mpaka 10 kucheua. Hivyo ni muhimu kuwapa ng'ombe wako muda wa kutosha wa kupumzika kwenye mazingira rafiki kwao.

6. Hakikisha unabadilisha chakula cha ng'ombe taratibu.

Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ni ngumu sana kuwa na upatikanaji wa malisho ya aina Moja mwaka mzima, kwakuwa ng'ombe wanahitaji chakula kila siku, wafugaji wengi huwapatia malisho tofauti tofauti kulingana na upatikanaji wa hayo malisho. Lakini sio salama haswa kwa ng'ombe wa maziwa kubadilishiwa chakula ghafla kwani inachukua muda mrefu kwa bacteria wa tumboni kuzoea mabadiliko ya ghafla na chakula kwahiyo huathiri mfumo mzima wa mmeng'enyo wa chakula hivyo huathiri moja kwa moja uzalishaji wa maziwa.

Mkulima anatakiwa kubadili chakula taratibu kwa kupunguza kidogo kidogo chakula alichozoea na kuongeza taratibu taratibu chakula kipya kabla ya kubadilisha kabisa angalau ndani ya wiki mbili ili aweze kuzoea, hii haitaathiri uzalishaji wake wa maziwa na ataendelea kutoa maziwa mengi siku zote.

7. Ukamuaji wa maziwa



Kwanza inatakiwa kuwe na sehemu maalumu lililotengwa kwa ajiri ya kukamulia maziwa, ng'ombe hawatakiwi kukamuliwa sehemu ambayo wanakaa mda ote kwani huweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kwa ng'ombe.  Pia ng'ombe wanatakiwa wapelekwe kwenye sehemu yakukamulia bila kupigwa pigwa kwani husababisha msongo wa mawazo ( Stress) hivyo huathiri utoaji wa maziwa, ni vizuri pia ng'ombe akiwa anakamuliwa maziwa awekewe viburudisho kama vile vyakula vya nyongeza ( Concentrate), mziki, kumuimbia, kumpigia miruzi  au malisho yoyote yale hii humfanya ng'ombe ajiachie ( Relax) hivyo huruhusu maziwa mengi yatoke wakati wa kukamuliwa.

Pia ni muhimu kusafisha chuchu kabla na baada ya kukamua maziwa, kuzipaka kilainishi kama vile mafuta Ili kupunguza msuguano wakati wa kukamua ( Endapo ng'ombe watakamukiwa kwa mkono), pia kuwapaka dawa maalumu kwa ajiri ya kuua bakteria ( Disinfectant) ambao husababisha maambukizi katika kiwele ( Udder) ambao huathiri afya ya ng'ombe na uzalishaji wa maziwa kwa ujumla.

Asante sana kwa kufuatilia makala hii.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana nasi kwa;

Barua pepe: info@agroottomans.com

 Imeandaliwa na: Husna Issa ( Agro economist)

 

Post a Comment

9 Comments