Kuna mwanasayansi mmoja Albert Eistein ( aliegundua bomu la nyuklia) alishawahi kusema " Kama huwezi elezea kitu kiuraisi basi haukifamu". Njia nyepesi kabisa ya kuelezea maana ya mfumuko wa bei ni neno " VYUMA VIMEKAZA" . Ukisikia mtu anasema hivi hii ndio mfumuko wa bei. Lakini kabla hatujaenda uko naomba nikurudishe nyuma kidogo tujadili pamoja kuhusu PESA.
Ivi umeshawahi kujiuliza pesa ni nini ?? Ilitoka wapi?? Pesa ilianzaje kutumika ? Ni nani ama taasisi gani inatengeneza pesa nchini ? Na ni kwa kiwango gani inazitengeneza??
Kwanini ufanye kazi kwa jili ya pesa wakati watu wanakaa wanazitengeneza ?? Na kama ni watu ni watu gani.?
Pesa ni mfumo wa kubadilishana kitu chenye thamani ambayo hukubalika na jamii fulani.Nchi ya kwanza duniani kuanza kutumia Pesa ( sarafu) ni China mnamo mwaka 770 kabla ya Kristo na ni mwaka 640 KK ndio pesa ya kwanza kwa maana ya noti( fiat money ) ilianza kutumika China. Kabla ya hapo watu walibadilishana vitu kwa vitu ( barter trade) ,kulingana na uhitaji ama umuhimu wa kitu kwa muhitaji husika.Katika historia kuna Vito vingi vimewahi kutumika kama pesa yani kama dhahabu, madini ya fedha(silver),chuma,shaba na kadhalika. Vitu hivi havikudumu sana kulingana na uzito ama ugumu na usalama wa kuvitunza. Dola ama serikali tofauti tofauti ndizo huwa na mamlaka ya kutengeneza fedha, hili lipo tangu kale .Kuna historia nyingi kwa namna pesa ilivyo anza kutumika .Japo nyingine hukinzana .Moja kati ya hizo ni hii apa; Mwanzoni katika historia dhahabu ilitumika kama pesa kulingana na mafikirio ya watu juu ya uthamani wake ( perceived value).( Hii inamaanisha dhahabu ina thamani kwa sababu tumeamini kuwa inathamani , tungeweza kuamini hata kitu kingine na kikatumika kwa namna ile ile )Lakini ilikuwa ngumu kutembea na dhahabu nyingi hivyo dhahabu ikawa inahifadhiwa ( kama vile benk) alafu mahali wanapohifadhi wanakupa karatasi inayo onesha kuwa wewe unadhahabu na hiyo karatasi unaweza itumia kununua kitu kulingana na dhahabu ulionayo. Hii inamaanisha nchi ilikuwa na ruhusa ya kutengeneza pesa kulingana na kiasi cha dhahabu inayomiliki( gold standard). Kumbe mpaka hapa umefahamu kuwa ni nchi kupitia benki kuu ya nchi husika ndio inayotengeneza pesa . Lakini je ni kwa kiasi gani benki kuu inaweza tengeneza pesa ?? Hapo zamani pesa ilitengenezwa kulingana na kiasi cha dhahabu inayomiliki ,ila kwa sasa serikali husika huamua kiasi cha pesa hizi . Hapa ndio shida zinapoanzia . Serikali nyingi hutumia " Modern monetary theory " kutengeneza pesa .
"Hii ina maanisha serikali inaweza kutengeneza pesa ama kuingiza pesa kwenye mzunguko ( printing money) kulingana na kiasi cha ukuaji wake wa uchumi."
Jambo hili ni sawa kwa kuwa kama nchi inakuwa kiuchumi maana yake kuna uzalishaji mpya wa bidhaa na huduma , ambazo zitahitaji pesa mpya ya kuzinunua . Kwakua hizo bidhaa hazikuwepo kabla.
Swali linakuja je ni kweli nchi huwa zinafanya hivi ? Jibu ni hapana .Kama umejifunza kitu hapo turudi kwenye mada yetu ya awali turudi sasa.
MAANA HALISI YA MFUMUKO WA BEI
Kupanda kwa wastani wa bei ya bidhaa na huduma ndio mfumuko wa bei . Hapa hatuongelei bidhaa moja ama mbili ni zaidi ya bidhaa 100 huangaliwa . Na katika hili kuna baadhi ya bidhaa ambazo huwa hazihusiki kupima mfumuko wa bei . Mfano wa bidhaa hizi ni kama bidhaa zote zilizopo katika soko la hisa ( financial markets), bidhaa ama huduma ambazo sio za lazima ( luxury goods) ama bidhaa zinazohusu matumizi ya serikali( government spending ).
SABABU ZA MFUMUKO WA BEI
Makala nyingi za uchumi zinanakiliwa zikisema mfumuko wa bei husabishwa na sababu kuu mbili
A) kuongezeka kwa ghalama za uzalishaji ( cost push)
B) kuogezeka kwa uhitaji ( demand pull)
Hii inaamaanisha kama ghalama za uzalishaji zitaongezeka basi moja kwa moja ghalama za bidhaa ziatongezeka na kama uhitaji wa bidhaa utaongezeka basi moja kwa moja wauzaji wa bidhaa hizo wataongeza bei kwa kuwa wanaoziitaji ni wengi .
Hili linaweza kuwa na ukweli ndani yake lakini swali ni je inakuwaje ghalama za uzalishaji zinaongezeka ghafla ama inakuwaje uhitaji ( public spending) wa zaidi ya bidhaa 100 unaongezeka gafla??
UHALISIA KUHUSU MFUMUKO WA BEI ?
Hili halipendwi sana kuongelewa na wachumi wengi ila ukweli ni kwamba sababu ya msingi ya mfumuko wa bei ni matumizi makubwa ya serikali kuliko mapato yake " too much government spending " pengine umeshtuka kidogo.
Sababu za ghalama na uhitaji sio chanzo cha moja kwa moja ( cost push and demand pull are secondary initiatives not primary cause) . Utakaposema mfumuko wa bei unasababishwa na ongezeko la uhitaji . Ntakuuliza hao watu wametoa wapi hizo pesa wanaotaka kuzimtumia??.Serikali ikiwa na matumizi makubwa mfano inatengeneza sana miundo mbinu kuliko ukuaji wake wa uchumi hizi pesa zitaenda mikononi mwa watu, zikienda mikononi mwa watu kila mtu atakuwa na pesa . Maanayake pesa itapatikana kiurahisi na kila mtu akitaka kuitumia basi bei za bidhaa zitapanda na mfumuko wa bei utatokea .
Hapa sasa nikuelezee kidogo alichokifanya Mansa Musa. Kwa kuwa huyu alikuwa tajiri mkubwa kipindi anaenda Maka kuhiji alipopita Misri aligawa dhahabu nyingi sana mtaani kwa maskini kama msaada. Na kipindi hicho dhahabu ilitumika kama pesa. Hii ilifanya kila mtu awe na dhahabu hivyo ikakosa thamani . Kwakua kila mtu alikuwa anaweza kununua anachotaka. Hii ikapelekea mfumuko wa bei ( demand pull inflation)
JINSI AMBAVYO SERIKALI INAWEZA SABABISHA MFUMUKO WA BEI.
Njia kuu ya serikali kujipatia mapato ni kukusanya kodi. Lakini kuna njia nyingine kama misaada, kukopa ama kutoa hati fungani . Serikali inapokuwa inaingiza pesa kwenye mzunguko huzitoa kwenye vyanzo kama hivi. Nadhani huwezi kuongelea kuhusu mfumuko wa bei bila kuitaja nchi ya Zimbambwe . Baada ya serikali kutengeneza pesa nyingi kuliko ukuaji wa uchumi matokeo yake vitu vilipanda bei kiasi kwamba mtu anaenda sokoni na tolori la pesa. Kwa sasa Zimbambwe asilimia za mfumuko wa bei ni zaidi ya 240% ( hyper Inflation)
Ili tuweze kufahamu namna serikali inavyoweza sababisha mfumuko wa bei pindi ikikiuka mifumo ya sheria za uchumi hapa tuzungumzie swala la Marekani. Mwaka 2020 baada ya homa ya Uviko 19 kutokea, Kulitokea kupungua kwa shughuli za kiuchumi ( global economic contraction) . Serikali ya Marekani iliamua kutengeneza pesa ( printing money ) na kuziweka kwenye mzunguko ili kwanza kuongeza matumizi ya watu( increase public spending) hili lingefufua uchumi sababu ya uhitaji wa bidhaa na pili lingesaidia biashara zipate mitaji. Katika kutimiza hili Benki kuu ya marekani ilipunguza ghalama ya kukopa fedha ( interest rate ) hadi asilimia 0.2 . Kwa namna hii pesa ilikua inapatikana kiurahisi sana . Ndani ya miezi mitatu serikali ya marekani iliingiza kiasi cha dolla za marekani Trillioni tatu kwenye mzunguko kama kichocheo cha kukuza uchumi( economic stimulus) kiasi hiki ni sawa na kiasi kilicho ingizwa kwa miaka minne ila kiliwekwa katika mzunguko kwa miezi mitatu tu.
Kwa miaka miwili ya mwanzo hili jambo halikuwa na shida kabisa . Ila kilicho onekana ni ukuaji wa thamani za soko la hisa kwa 20%. Kwakuwa soko la hisa halitumiki kupima mfumuko wa bei marekani iliona hili jambo ni sawa. Madhara yake yamekuja kutokea mwaka uliofata 2022 ambapo mfumuko wa bei umepanda kwa zaidi ya 10%( kiasi hiki hakijawai kutokea tangu vita ya pili ya Dunia) , asilimia ya wasiojiliwa Marekani( unemployment rate)imepanda hadi 14% na mwaka 2023 mwezi wa nne Benki kubwa tatu za Marekani zimefilisika ikiwemo Sillicon Valley Bank ambayo ilikuwa ni ya 16 kwa ukubwa Marekani. Huu ni mfano wa kuongeza uhitaji( Demand pull inflation ) . Kama serikali itaamua kuzalisha ama kukopa pesa kiholela bila kuangalia ukuaji wake wa uchumi basi inaweza kupelekea mfumuko wa bei.
Tulisema kuwa kuna aina nyingine ya mfumuko wa bei inayoweza kusababishwa na kuongezeka kwa ghalama za uzalishaji. Njia nyepesi ya kuongezeka kwa ghalama za uzalishaji ni kuongezeka kwa kodi . Kama bidhaa mama amabazo zinatumiwa na watu zitaongezewa kodi basi ghalama za uzalishaji zitaongezeka hii hali husababisha ongezeko la bei. Ndio maana serikali ya Tanzania hutoa ruzuku ya mbolea na viatilifu ili kupunguza ghalama ya kulima mazao ya chakula kuzuia mfumuko wa bei wa bidhaa hizo ambao unaweza enea hadi kwenye bidhaa nyingine.
NAMNA GANI BIDHAA ZA MAFUTA ( PETROLIUM PRODUCT) HUSABISHA MFUMUKO WA BEI.

Tumejifunza hapo mwanzo kuwa sababu moja ya mfumuko wa bei ni kuongezeka kwa ghalama za uzalishaji. Bidhaa za mafuta ni chanzo cha nishati kwa karibia kila aina ya uzalishaji. Kama mafuta yanaongezeka bei basi ni rahisi sana kwa bei za bidhaa kupanda. Mfano mzuri ni swala lililotokea Ujerumani mwaka 2022 na 2023. Kutokana na vita ya Urusi na Ukraini Urusi imepunguza kiwango cha mafuta yanayoenda Ujerumani. Na uchumi wa Ujerumani unategemea zaidi uzalishaji . Hili limekuwa moja ya sababu kufanya uchumi wake kuzorota ( recession). Kama kodi inayotozwa kwenye mafuta na nchi husika ikiongezeka basi hili linaweza pelekea mfumuko wa bei .
ATHARI ZA MFUMUKO WA BEI KIUCHUMI
Athari kubwa ya mfumuko wa bei ni kupunguza uwezo wa pesa kununua bidhaa( decresed in consumers purchasing power). Kama uwezo wa pesa wa kununua bidhaa umepungua itakuwa ghali hasa kuagiza bidhaa nje ya nchi. Itabidi nchi kutumia pesa nyingi zaidi kuagiza kitu kile kile .
Lakini kwa kuwa kipindi chote cha mfumuko wa bei ni lazima benki kuu kuongeza Vizio ama asilimia ya kurudisha pesa ( interest rate ), hii inapelekea waliokopa warudishe pesa nyingi zaidi kuliko ilivokuwa awali . Hii inafanya maisha yawe magumu zaidi. Na kwanini nilisema neno "vyuma vimekaza " ndio maana halisi ya mfumuko wa bei ? Kama wewe ni muajiriwa na ulikuwa unapokea mshahara laki 5. Na ulikuwa unatumia laki 2 kwa chakula . Kipindi mfumuko wa bei ukiongezeka mshahara wako utabaki vile vile laki 5 , alafu chakula inabidi ununue lak 3 . Hapo utachagua mawili . Aidha upunguze matumizi yasio ya lazima ama upunguze kiasi cha chakula kwa familia yako. Kama matumizi yote ni ya lazima itabidi ukope ili uishi . Hapo ndo lazima uone vyuma vimekaza.
JE INAWEZEKANA KUKAWA HAKUNA KABISA MFUMUKO WA BEI ?( zero inflation rate)
Hali hii kiuchumi sio nzuri na nikazi kuifikia. Kama bei za vitu hazipandi kabisa inamaanisha pesa haipungui thamani yake . Na kama pesa haipungui thamani yake watu hawapati motisha kuitumia na kama watu hawatumii pesa maana yake bidhaa hazita pata wateja na bidhaa zikikosa wateja inamaanisha uzalishaji utapungua na uzalishaji ukipungua uchumi utazorota. Wachumi wengi huwa wanakubaliana mfumuko wa bei kwa asilimia 2 hadi 3 ni mzuri kufanya uchumi uweze kukua zaidi
UWEKEZAJI UPI NI SALAMA KIPINDI CHA MFUMUKO WA BEI??
Kwa watumiaji mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma lakini kwa muwekezaji hiki ni kipindi cha kupata faida zaidi .Hii ni kwa sababu mara nyingi ongezeko la bei huwa kubwa kuliko ongezeko la ghalama za uzalishaji. Lakini kwa kuwa tumesema kipindi cha mfumuko wa bei pesa inapoteza uwezo wake wa kununua kumbe kama mfanyabiashara ama mtu yoyote kutunza pesa benki kipindi cha mfumuko wa bei ni tatizo kubwa . Kwakuwa utakuwa na makaratasi mengi yasio na thamani . Wengine wanadhani pengine waweke ( fixes account) . Swali ni je benki inaweza kukupa faida kuliko ongezeko la uchumi ?? Jibu ni hapana . Kama Benki kubwa kama Silicon Valley ya Marekani ina feli . Hizi benki zetu je ??
Kipindi cha mfumuko wa bei inatakiwa uwekeze kwenye vitu vinavyopanda bei( raising asset) .Mfano wa vitu hivyo ni kama Hisa za makampuni ya vitu vya muhimu kwa matumizi ya watu kama vile chakula ,nishati, hati fungani za serikali, baadhi ya bidhaa kama dhahabu ama madini ya fedha(Silver)hupanda thamani. lakini hisa ama bidhaa hasa zinazouzwa kama vitu vya ziada kama ( pombe, baadhi ya vitu vya starehe ama visivyo vya lazima ) hushuka thamani. Kitu kikubwa cha kuondoka nacho hapa ni kwamba kipindi cha mfumuko wa bei hasa hiki cha mwaka huu pesa inapoteza uthamani wake kwaio usitunze pesa nyingi tunza vitu . Sababu vitapanda bei . Nunua hata shamba , ama kiwanja ama mifugo . Ila usinunue vitu vinavyoshuka thamani ( liability) .nununa vitu vinavyopanda thamani (asset )
NJIA SERIKALI INAYOTUMIA KURATIBU MFUMUKO WA BEI
Kuna njia kuu mbili serikali hutumia kuratibu mfumuko wa bei .
A) kupitia benki kuu( monetary policy)
B) kupitia bunge ( fiscal policy)
A) kupitia benki kuu.
Hii ni njia ambayo serikali hupunguza kiasi cha pesa kwenye mzunguko. Hii hutokea pale mfumuko wa bei unapotokea, kunakuwa na pesa nyingi mikononi mwa watu ( too much money chasing few goods) . Kwaio njia pekee ni ya kuirudisha pesa mikononi mwa serikali . Hili linafanyika kwa kwanza benki kuu kuongeza riba ya kukopa pesa kwa benki na taasisi za fedha ili kufanya watu wasichukue mikopo kiurahisi , pia hutoa hati fungani ( government bond) ili pesa iwepo mikoni mwa serikali .
B) kupitia Bunge
Hii ni njia ambayo serikali hutumia kodi na matumizi ya serikali kupunguza pesa kwenye mzunguko. Tulisema mfumuko wa bei husababishwa na uhitaji mkubwa wa bidhaa ( demand pull). Njia ya kwanza serikali ni kuongeza kodi ili kufanya uhitaji wa bidhaa upungue . Lakini pia tulisema sababu nyingine kubwa ya mfumuko wa bei ni matumizi makubwa ya serikali .hivyo serikali ikipunguza matumizi basi pesa hupungua kwenye mzunguko.
JE SERIKALI INAWEZA KURATIBU MFUMUKO WA BEI KWA UFANISI?
Jibu ni hapana . Serikali haina uwezo wa kuratibu mfumuko wa bei kwa ufanisi . Hili ni kwa sababu ya kuu mbili.
1. Ili serikali iweze kuainisha kuwa kuna mfumuko wa bei wa asilimia kadhaa inahitaji kutumia wachumi kufanya utafiti . Mpaka wachumi wapate majibu pengine mfumuko huo wa bei umeshaondoka ama umeongezeka ama umepungua , hivyo ufanisi wa kuzuia ama kuratibu ni lazima uwe mdogo. Kitaalamu wanaita "time lag". Hata kwa mfumo wa bunge hadi litoe maamuzi ya kuongeza ama kupunguza kodi muda huo mfumuko wa bei utakuwa umebadilika
2.Njia moja wapo ya serikali kuzuia mfumuko wa bei ni kupunguza matumizi. Shida ya njia ni kwamba ile pesa iliotunzwa ni lazima mwaka unao fata serikali ipate matumizi tu ya kuitumia.
Japokuwa serikali haiwezi kuzuia mfumuko wa bei kwa ufanisi lakini haiwezi kuacha tuu bei zipande . Lazima ifanye kitu .
Kwakuwa tunaishi katika ulimwengu wa utandawazi uchumi wa nchi moja unaweza athiri uchumi wa nchi nyingine . Sio kila mfumuko wa bei unasabishwa na matumizi makubwa ya serikali . Meingine hutokana na vitu vilivyo juu ya uwezo kama mabadiliko ya bei za nishati kwenye soko la dunia .( ongezeko la bei za mafuta) Sababu kama hizi wakati mwingine ni ngumu kuzizuia japo nchi kubwa kama Marekani hutunza mfano mafuta kama akiba ili yatumike kipindi bei za dunia zikiwa zimepanda kama hivi sasa.
KILIMO BIASHARA NA MFUMUKO WA BEI.

Kama nilivyo eleza hapo awali si kila bidhaa huwa inapanda bei kipindi cha mfumuko wa bei. Hili ni sawa hata katika bidhaa za kilimo. Kipindi hiki ni zile bidhaa za msingi tu ambazo mara nyingi hupanda kwa kuwa watu hubadili zaidi matumizi yao . Kwa kawaida bidhaa mama za chakula ( neccesity agri produce) kama mahindi , mchele , maharage, mihogo ama alizeti hupanda bei .Lakini bidhaa za chakula ambazo si za msimgi sana ( luxury agri produce) kama vanilla, korosho , viungo ama ubuyu hizi mara nyingi hushuka bei . Lakini kupanda ama kushuka bei kwa bidhaa za kilimo hutokana na sababu nyingine nyingi kama uzalishaji kwa mwaka huo, uhitaji wa soko la dunia, msimu ama eneo husika.
Bila shaka umejifunza kitu.
Ubarikiwe sana.
Makala hii imendikwa baada ya kuulizwa maswali mengi hasa na mdogo wangu Agustino Kimwaga.Wasiliana nasi kupitia:
+255744207795
Erick Muhini ( Agro Economist )
2 Comments
hauna kundi la whatsapp tulipie kwa ajili ya elimu zaidi ,nimejifunza
ReplyDeleteAsante kwa kutufuatilia kwa sasa hatuna kundi ila unaweza kujisomea makala zote bure kwenye blog na app yetu
Delete